Friday, 30 September 2016

BARAKA YA YUDA





Baraka ya Yuda iko ndani ya Jina Lake. Neno Yuda Linalotokana na neno la Kiebrania yadah. Yadah maana yake ni “kustahi au kunyoosha mikono” “kukiri”, “kusifu” au “kutoa shukrani”. Jina la Yuda linamaanisha sifa. Kwa nini hii ni baraka? Kwa sababu sifa ndicho kivutio pekee kinachopelekea uwepo wa Mungu kwetu.

Mwanzo 29:35 "Akapata mimba tena, akazaa mwana. Akasema, Mara hii nitamsifu Bwana; kwa hiyo akamwita jina lake Yuda; akaacha kuzaa."

Sifa ni dawa ya Mungu ibadidirishayo Mazingira yako.
Lea angeweza kuchagua Mazingira yake, na angechagua jina ambalo hata lisingeleta baraka kwake. Elewa kabisa alikuwa hapendwi na Yakobo, alimpenda mdogo wake Raheli kuliko Lea.
Maisha ya Lea yalikuwa ya mateso sana, Mungu akaonesha rehema zake na akamruhusu Lea kuzaa watoto wakati Raheli alikuwa hazai.
Mwanzo 29:31 "Bwana akaona ya kwamba Lea hakupendwa, naye akafungua tumbo lake; bali Raheli alikuwa hazai."

Hata hili halikusababisha Yakobo kumpenda Lea. Baada ya kumpa mwanae wa kwanza jina la Reubeni-Kwa kuwa Bwana ameona teso langu (Mwanzo 29:32) –na mwana wa pili akamwita Simeoni (Mwanzo 29:33)-kwa kuwa Bwana amesikia mimi sikupendwa. Lakini Lea alipopata mtoto wa tatu Akampa jina la Yuda 
“Mwanzo 29:35 Akapata mimba tena, akazaa mwana. Akasema, Mara hii nitamsifu Bwana; kwa hiyo akamwita jina lake Yuda; akaacha kuzaa”

Bwana alifurahishwa na jina ambalo Lea alichagua kwa mtoto wake Yuda (Tazama Zaburi 78:67-68). Mungu alichagua Yuda kupokea baraka na kuwa babu wa Mfalme Daudi na Masihi

1 Mambo ya Nyakati 28:4 "Walakini Bwana, Mungu wa Israeli, alinichagua katika nyumba yote ya babangu kuwa mfalme juu ya Israeli milele, kwa kuwa amemchagua Yuda awe mkuu; na katika nyumba ya Yuda, alichagua nyumba ya babangu, na miongoni mwa wana wa babangu, aliniridhia mimi ili kunitawaza niwe mfalme juu ya Israeli wote;"

Umuhimu wa kabila la Yuda umeonekana katika Agano la kale maana walikuwa viongozi na hii baraka alitoa Yusufu alipobariki wanawe (Mwanzo 49:8-12)
Na uongozi wa kabila la Yuda pia unaonekana katika kitabu cha Waamuzi wakati makabila ya Isaraeli yanaenda vitani dhidi ya kabila la Benjamini, Mungu anaagiza kabila la Yuda liongoze vita (Waamuzi 20:18)
Baada ya kutoka utumwani katika kuweka wakfu ukuta wa Yerusalemu Bwana akaweka kwaya mbili za kabila la Yuda (Nehemia 12:27-31)
Katika Zaburi 108:8 Yuda ameelezewa kama Fimbo ya Mungu. Hapo inamaanisha Yuda ni mwakilishi wa mamlaka na nguvu ya Mungu. Na hili lilitimizwa na mfalme Daudi na waliofuatia kwake na zaidi sana Yesu Kristo.
Katika agano Jipya mamlaka ya Mungu alifunuliwa na uzao wa kabila la Yuda -
Ufunuo wa Yohana 5:5 "Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba."

Na hata Ufunuo 7:5 tunaona watatiwa Muhuri kwanza kabila la Yuda nyakati za Mwisho.
Kibali cha Mungu katika uzao wa Yuda tunaona pia 

Zaburi 114:2 “Yuda ilikuwa patakatifu pake, Israeli milki yake.” 

Kwa maana nyingine Mungu alionesha mamlaka yake na nguvu zake kwa Waisreali wote ila makao makuu yake na makazi yake ya kuishi yalikuwa Yuda.
Yuda iliona uwepo wa Mungu wa pekee sana kuliko kabila lolote. Yerusalem na mlima Sayuni, mlima ambapo hekalu lilisimamishwa ilikuwa ndani ya mipaka ya Yuda

Zaburi 76:1-2 “Katika Yuda Mungu amejulikana, Katika Israeli jina lake ni kuu. Kibanda chake pia kiko Salemu, Na maskani yake iko Sayuni.”

Yuda ililindwa na Mungu sana kwa sabubu ndipo palipokuwa mahali pa uwepo wake.

Na; Pastor Boniface Evarist
Efatha Ministry - Mbinga. 

No comments:

Post a Comment