Maarifa yana nafasi kubwa sana kubadili maisha yako, msingi wa maisha yako na mafanikio yake iwe Kiroho, Kiuchumi, Kifamilia, Ndoa, Kazi yako au jambo lolote lile hutegemea sana maarifa uliyonayo katika jambo hilo, epuka kuhifadhi taarifa zisizo sahihi kwani zitafanyika uharibifu kwako. Kwa gharama yoyote ile hakikisha unahifadhi taarifa chanya na achana na taarifa hasi, epuka ushauri wa walioshindwa na kukata tamaa, na jifunze kwa waliofanikiwa katika changamoto na kutimiza malengo na maono waliyonayo.
MAHUSIANO YALIYOPO KATI YA IMANI NA MAARIFA.
Kama tulivyojifunza toka katika toleo lililopita kuwa; Maarifa ni uhalisia, taarifa na ujuzi anaoupata mtu kupitia uzoefu au elimu; ni dhahania au kwa kulitenda jambo. Pia maana ya Imani kama ilivyoelezwa ki-Biblia;
Waebrania 11:1 "Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana"
Imani ni sehemu ya maarifa aliyonayo mtu, kwani katika maarifa tunaona neno DHAHANIA, ambapo katika Waebrania linaelezwa kama mambo yanayotarajiwa na mambo yasiyoonekana.
Imani ya mtu inategemea sana maarifa aliyonayo, kwani Imani hutokana na kile ambacho ufahamu wa mtu umekipokea yaani maarifa aliyonayo. tunasoma;
Warumi 10:17 "Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo."
Hii inaonyesha kuwa ili mtu aweze kuamini, lazima apate maarifa ya kumuwezesha kuamini. Huwezi kuamini kitu ambacho hakipo akilini mwako, ndio maana mtu ili aamini, anahitaji aisikie Injili ya Neno la Kristo ili apate kuamini, tunasoma;
Marko 16:15-16 "Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa."
Tumeona Ki-Biblia Mahusiano yaliyopo kati ya Maarifa na Imani, Kweli isiyofahamika kwa mtu; mtu huyo hawezi kuiamini, kwani ni kitu ambacho hakipo kabisa katika ufahamu wake. Pia kupata maarifa na kuamini ni vitu viwili tofauti, kwani wengine hupata maarifa lakini mioyo yao haipo tayari kuamini. Unaweza kukutana na mtu anayafahamu maandiko ya kwenye Biblia vizuri sana, ila hakuna anachoamini toka katika maandiko hayo ya kwenye Biblia.
Mathayo 13:14-15 "Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona. Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya."
Tunaona dhahiri katika mtiririko huu kuwa kuna hatua ya kusikia na kuona ambayo ni sawa na kupokea maarifa, lakini hatua ya kuongoka ambayo ni matokeo ya kuamini kilichosikiwa au kilichoonwa.
Imani ni kweli, thabiti, hivyo imani yako ili isiwe potofu ni lazima iwe KWELI. Kwani kama mtu ameamua kuamini kitu au jambo ambalo si kweli, imani hiyo huitwa imani potofu.
~ BARIKIWA SANA!! ~
Kwa maoni au ushauri wasiliana nami; agreyndiwu@gmail.com Simu; +255 71 346 9596
No comments:
Post a Comment