Wednesday, 27 April 2016

MAMBO MUHIMU KATIKA KUFIKIA MAFANIKIO ~ TOLEO MAALUMU



Ni miaka nane sasa tangu niokoke na kujiunga na kanisa la Efatha tarehe 27 Aprili 2008. Sijawahi kujutia maamuzi haya, zaidi sana naona kuwa bado sijafikia viwango nilivyokusudiwa. Nakaza mwendo nifikie viwango nilivyokusudiwa ili nipate kutimiza kusudi la kuumbwa kwangu. Leo napenda kuwashirikisha mambo yafuatayo ambayo ni muhimu kuyatambua katika kufikia mafanikio yako;

1.      KUWATAMBUA WATU SAHIHI KWAKO;
Kuna watu ambao unaweza kutana nao katika maisha yako, ukawaona kuwa ni watu muhimu sana na kiukweli wakafanyika msaada kwa namna moja au nyingine katika maisha yako, lakini watu hao hao wakafanyika uharibifu mkubwa sana.
Kumbuka kuwa shetani anapotaka kukuangamiza hatokuja na mambo mabaya tu, atakuletea mambo mazuri lakini ndani yake anachanganya na uharibifu kwa ajili ya kukuangamiza. Kuwa makini sana na watu wa aina hii, watu hawa ndio wale wanaotamkwa kuvaa ngozi ya kondoo wakati ndani yao ni mbwa mwitu. Mwombe Mungu akukutanishe na watu sahihi kwako.

2.      KUWEKA MATUMAINI MAHALA SAHIHI;
Matumaini yako; hiki pia ni kipengele muhimu sana, lazima ujue ni nani unamtumainia katika maisha yako. Kuwatumainia wanadamu hata kama wanamsaada mkubwa sana katika maisha yako ni kutafuta mauti yako, kumbuka umeumbwa na Mungu kwa kusudi lake, hivyo basi Mungu hahitaji kutafutiwa watu wa kumsaidia kutimiza kusudi lake, yeye anao wengi. Hata katika maisha yako, si wewe unayemtumia Mungu kutimiza kusudi lako, bali ni Mungu anakutumia wewe kutimiza kusudi lake. Biblia pia inasema amelaaniwa mtu Yule amtegemeaye mwanadamu na amebarikiwa mtu Yule amtegemeaye Bwana.

3.      KUJIAMINI;
 Kutojiamini na kutothubutu, kipengele hiki ni kibaya sana, kwani hata kama una uwezo mkubwa kiasi gani, endapo utakosa kujiamini nma kuthubutu hakuna kitu kitatokea katika maisha yako. Kutojiamini ni sawa na kuwa na risasi pasipo bunduki, na kutothubutu ni sawa na kuwa na risasi na bunduki lakini kutofyatua risasi ili kusababisha jambo litokee.

4.      KUWA NA MAARIFA;
 Watu wengi sana wamekuwa wavivu wa kutafuta maarifa, hupenda sana wengine wawatafutie taarifa na kuwasimulia. Kamwe hutoendelea kwa kutegemea wengine wakutafutie taarifa na kukusimulia. Huwezi kukua kiroho kwa kusubiri Mchungaji wako au kiongozi wako yeyote wa kiroho akusomee Biblia siku za Ibada na kukutafsiria, ni lazima uchukue hatua wewe mwenyewe ya kumtafuta Mungu kwa juhudi. Wengine pia wanaona njia rahisi ni kukimbilia kusoma vitabu vilivyoandikwa na watumishi mbali mbali hasa vikiwa na kurasa chache kwa sababu ya uvivu wa kusoma Biblia yenye vitabu vingi. Huwezi kukua kwa staili hii, kwani si kila kitabu kilichoandikwa na mtumishi wa Mungu kipo sahihi, ni kwa wewe mwenyewe kuchukua hatua ya kusoma Biblia na kumwomba Roho Mtakatifu akusaidie ndio itakupa ufahamu wa juu. Hata utakaposoma vitabu mbalimbali vya watumishi, utaweza kutambua sehemu ambazo hazijaandikwa kwa usahihi.
Katika jambo lolote, tafuta maarifa wewe mwenyewe, usisubiri kusimuliwa na wengine, chukua hatua.

5.      KUPENDA URAHISI/UVIVU;
Kupenda njia rahisi, watu wengi hupenda kupata mambo kirahisi rahisi, kumbuka kuwa umeumbwa kwa kusudi la Mungu, usiwe kigeugeu katika kulitimiza kusudi hilo, unaona ndani yako una wito wa kumtumikia Mungu, lakini ukiangalia mazingira unayaona magumu kwa macho yako ya klibinadamu na unatakata kuacha ili uende kwenye jambo jingine, jiulize hilo unalotaka kulikimbilia ni kusudi la nani? Mungu amekuita kwenye kusudi lipi? Usiutoroke wito ulioitiwa, kwani katika wito ulioitiwa utapaswa kutoa hesabu siku ya mwisho.

"Binafsi napenda kuwashukuru sana wale wote waliofanyika msaada kwangu kwa namna moja au nyingine,bado natambua sana mchango wenu kwangu, Wazazi wangu, Mwl. Athuman Z Ngonyani, Mr. & Mrs Kattanga, Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira na watumishi wote ndani ya Huduma ya Efatha, Uncle Gaston A. Nchimbi,Mr. Amon Mandele, Mr. John Sweke, Mr. Kachingwe Kaselenge, Ndugu zangu, jamaa na marafiki, natambua mchango wenu,  Mungu asiwapungukie kwa wingi wa baraka zake; Amina."

No comments:

Post a Comment