Wednesday, 27 April 2016

MAMBO MUHIMU KATIKA KUFIKIA MAFANIKIO ~ TOLEO MAALUMU



Ni miaka nane sasa tangu niokoke na kujiunga na kanisa la Efatha tarehe 27 Aprili 2008. Sijawahi kujutia maamuzi haya, zaidi sana naona kuwa bado sijafikia viwango nilivyokusudiwa. Nakaza mwendo nifikie viwango nilivyokusudiwa ili nipate kutimiza kusudi la kuumbwa kwangu. Leo napenda kuwashirikisha mambo yafuatayo ambayo ni muhimu kuyatambua katika kufikia mafanikio yako;

1.      KUWATAMBUA WATU SAHIHI KWAKO;
Kuna watu ambao unaweza kutana nao katika maisha yako, ukawaona kuwa ni watu muhimu sana na kiukweli wakafanyika msaada kwa namna moja au nyingine katika maisha yako, lakini watu hao hao wakafanyika uharibifu mkubwa sana.
Kumbuka kuwa shetani anapotaka kukuangamiza hatokuja na mambo mabaya tu, atakuletea mambo mazuri lakini ndani yake anachanganya na uharibifu kwa ajili ya kukuangamiza. Kuwa makini sana na watu wa aina hii, watu hawa ndio wale wanaotamkwa kuvaa ngozi ya kondoo wakati ndani yao ni mbwa mwitu. Mwombe Mungu akukutanishe na watu sahihi kwako.

2.      KUWEKA MATUMAINI MAHALA SAHIHI;
Matumaini yako; hiki pia ni kipengele muhimu sana, lazima ujue ni nani unamtumainia katika maisha yako. Kuwatumainia wanadamu hata kama wanamsaada mkubwa sana katika maisha yako ni kutafuta mauti yako, kumbuka umeumbwa na Mungu kwa kusudi lake, hivyo basi Mungu hahitaji kutafutiwa watu wa kumsaidia kutimiza kusudi lake, yeye anao wengi. Hata katika maisha yako, si wewe unayemtumia Mungu kutimiza kusudi lako, bali ni Mungu anakutumia wewe kutimiza kusudi lake. Biblia pia inasema amelaaniwa mtu Yule amtegemeaye mwanadamu na amebarikiwa mtu Yule amtegemeaye Bwana.

3.      KUJIAMINI;
 Kutojiamini na kutothubutu, kipengele hiki ni kibaya sana, kwani hata kama una uwezo mkubwa kiasi gani, endapo utakosa kujiamini nma kuthubutu hakuna kitu kitatokea katika maisha yako. Kutojiamini ni sawa na kuwa na risasi pasipo bunduki, na kutothubutu ni sawa na kuwa na risasi na bunduki lakini kutofyatua risasi ili kusababisha jambo litokee.

4.      KUWA NA MAARIFA;
 Watu wengi sana wamekuwa wavivu wa kutafuta maarifa, hupenda sana wengine wawatafutie taarifa na kuwasimulia. Kamwe hutoendelea kwa kutegemea wengine wakutafutie taarifa na kukusimulia. Huwezi kukua kiroho kwa kusubiri Mchungaji wako au kiongozi wako yeyote wa kiroho akusomee Biblia siku za Ibada na kukutafsiria, ni lazima uchukue hatua wewe mwenyewe ya kumtafuta Mungu kwa juhudi. Wengine pia wanaona njia rahisi ni kukimbilia kusoma vitabu vilivyoandikwa na watumishi mbali mbali hasa vikiwa na kurasa chache kwa sababu ya uvivu wa kusoma Biblia yenye vitabu vingi. Huwezi kukua kwa staili hii, kwani si kila kitabu kilichoandikwa na mtumishi wa Mungu kipo sahihi, ni kwa wewe mwenyewe kuchukua hatua ya kusoma Biblia na kumwomba Roho Mtakatifu akusaidie ndio itakupa ufahamu wa juu. Hata utakaposoma vitabu mbalimbali vya watumishi, utaweza kutambua sehemu ambazo hazijaandikwa kwa usahihi.
Katika jambo lolote, tafuta maarifa wewe mwenyewe, usisubiri kusimuliwa na wengine, chukua hatua.

5.      KUPENDA URAHISI/UVIVU;
Kupenda njia rahisi, watu wengi hupenda kupata mambo kirahisi rahisi, kumbuka kuwa umeumbwa kwa kusudi la Mungu, usiwe kigeugeu katika kulitimiza kusudi hilo, unaona ndani yako una wito wa kumtumikia Mungu, lakini ukiangalia mazingira unayaona magumu kwa macho yako ya klibinadamu na unatakata kuacha ili uende kwenye jambo jingine, jiulize hilo unalotaka kulikimbilia ni kusudi la nani? Mungu amekuita kwenye kusudi lipi? Usiutoroke wito ulioitiwa, kwani katika wito ulioitiwa utapaswa kutoa hesabu siku ya mwisho.

"Binafsi napenda kuwashukuru sana wale wote waliofanyika msaada kwangu kwa namna moja au nyingine,bado natambua sana mchango wenu kwangu, Wazazi wangu, Mwl. Athuman Z Ngonyani, Mr. & Mrs Kattanga, Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira na watumishi wote ndani ya Huduma ya Efatha, Uncle Gaston A. Nchimbi,Mr. Amon Mandele, Mr. John Sweke, Mr. Kachingwe Kaselenge, Ndugu zangu, jamaa na marafiki, natambua mchango wenu,  Mungu asiwapungukie kwa wingi wa baraka zake; Amina."

Saturday, 16 April 2016

NGUVU YA MAARIFA - SEHEMU YA PILI


 Maarifa yana nafasi kubwa sana kubadili maisha yako, msingi wa maisha yako na mafanikio yake iwe Kiroho, Kiuchumi, Kifamilia, Ndoa, Kazi yako au jambo lolote lile hutegemea sana maarifa uliyonayo katika jambo hilo, epuka kuhifadhi taarifa zisizo sahihi kwani zitafanyika uharibifu kwako. Kwa gharama yoyote ile hakikisha unahifadhi taarifa chanya na achana na taarifa hasi, epuka ushauri wa walioshindwa na kukata tamaa, na jifunze kwa waliofanikiwa katika changamoto na kutimiza malengo na maono waliyonayo.


MAHUSIANO YALIYOPO KATI YA IMANI NA MAARIFA.

Kama tulivyojifunza toka katika toleo lililopita kuwa; Maarifa ni uhalisia, taarifa na ujuzi anaoupata mtu kupitia uzoefu au elimu; ni dhahania au kwa kulitenda jambo. Pia maana ya Imani kama ilivyoelezwa ki-Biblia;

Waebrania 11:1 "Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana"


Imani ni sehemu ya maarifa aliyonayo mtu, kwani katika maarifa tunaona neno DHAHANIA, ambapo katika Waebrania linaelezwa kama mambo yanayotarajiwa na mambo yasiyoonekana.
Imani ya mtu inategemea sana maarifa aliyonayo, kwani Imani hutokana na kile ambacho ufahamu wa mtu umekipokea yaani maarifa aliyonayo. tunasoma;

Warumi 10:17 "Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo."

Hii inaonyesha kuwa ili mtu aweze kuamini, lazima apate maarifa ya kumuwezesha kuamini. Huwezi kuamini kitu ambacho hakipo akilini mwako, ndio maana mtu ili aamini, anahitaji aisikie Injili ya Neno la Kristo ili apate kuamini, tunasoma;

Marko 16:15-16 "Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa."

Tumeona Ki-Biblia Mahusiano yaliyopo kati ya Maarifa na Imani, Kweli isiyofahamika kwa mtu; mtu huyo hawezi kuiamini, kwani ni kitu ambacho hakipo kabisa katika ufahamu wake. Pia kupata maarifa na kuamini ni vitu viwili tofauti, kwani wengine hupata maarifa lakini mioyo yao haipo tayari kuamini. Unaweza kukutana na mtu anayafahamu maandiko ya kwenye Biblia vizuri sana, ila hakuna anachoamini toka katika maandiko hayo ya kwenye Biblia.

Mathayo 13:14-15 "Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona. Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya."

Tunaona dhahiri katika mtiririko huu kuwa kuna hatua ya kusikia na kuona ambayo ni sawa na kupokea maarifa, lakini hatua ya kuongoka ambayo ni matokeo ya kuamini kilichosikiwa au kilichoonwa.
Imani ni kweli, thabiti, hivyo imani yako ili isiwe potofu ni lazima iwe KWELI. Kwani kama mtu ameamua kuamini kitu au jambo ambalo si kweli, imani hiyo huitwa imani potofu.

~ BARIKIWA SANA!! ~
 Kwa maoni au ushauri wasiliana nami; agreyndiwu@gmail.com Simu; +255 71 346 9596

Thursday, 14 April 2016

KUSHINDA MAJARIBU


NA: MCHUNGAJI BONIFACE EVARIST.
        EFATHA MINISTRY - MBINGA

SOMO: KUSHINDA MAJARIBU II:
Majaribu ni sehemu ya utumishi.
Kupitia kwenye majaribu na mapito ni sifa ya mkristo aliyeokoka.
Ibada iliyopita tuliangalia sehemu ya kwanza ya somo hili, ambapo msingi wake ulitoka kwenye Yakobo 1:12 " Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao.
Majaribu tunayashinda kwa unyenyekevu.
Wokovu upo kwenye unyenyekevu.

Tunaanza sasa sehemu ya pili ya somo letu "KUSHINDA MAJARIBU"
Yakobo 4:7
"Basi mtiini Mungu. Mpingeni shetani, naye atawakimbia."

Mtu hujaribiwa na shetani, wala hajaribiwi na Mungu.
Yakobo 1:13; "Mtu ajaribiwapo, asiseme, Ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu."

Kujitiisha kunako kusudi la Mungu ni silaha ya kusababisha uweze kushinda majaribu na majaribio. Ni hekima kujitiisha mbele za Mungu.

For you to win against the temptations and trials, submit yourself to God. Surrender yourself to God.

Mkaribieni Mungu naye atawakaribia.
Ukimkaribia Mungu; kicheko, maarifa, hekima, shauri, nguvu ya uweza, ufahamu yaani roho saba zinakuwa nawe.
Unakuwa sumaku, ukimkaribia Mungu naye anakukaribia.
Lazima ufike mahali pa kujitiisha kwa Mungu, jisalimishe kabisa ili yeye akuongoze katika njia zako. Kinachomfanya mwanafunzi kufeli masomo ni kukosa kuzingatia.
Kinachomfanya mkristo kushindwa katika majaribu na mapito ni kukosa kuzingatia. Uwapo kanisani zingatia ili ujitiishe.
JITIISHE KWA MUNGU ILI KUSHINDA MAJARIBU.
Kama hushindi majaribu na mapito, utachelewa sana kumwona Mungu.
Furahia majaribu na mapito maana ukiyashinda utawahi kumwona Mungu katika maisha yako.
MAJARIBU NA MAPITO NI SIFA YA UTAKATIFU WAKO.
Dhambi uliyokuwa unaifanya kabla ya kuokoka ndio itakayokuwa jaribu kwako.
Tafuta kujua lugha ya kila jambo ili kushinda majaribu.
Yesu Kristo ni rafiki wa karibu sana wakati WA majaribu. Ili kufurahia uwepo wake twatakiwa kumtii Mungu, na kumpinga shetani ili atukimbie kabisa.
Kinachofanya tusione faida ya wokovu wetu wakati WA majaribu no kiburi na fahari. Biblia inasema 'kiburi hupelekea anguko'
OMBA HIVI:
Bwana Yesu, najitiisha kwako, naomba niondolee kiburi, nitii neno lako.
Rum 13:3(b)
"......... Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya mema, nawe utapata sifa kwake."
Tukitenda mema hatutamwogopa Mungu mwenye mamlaka yote.
Anayetushindia majaribu ni Roho Mtakatifu.
ILI KUSHINDA MAJARIBU, TUNAHITAJI MAMBO MAWILI:
1. Unyenyekevu (humility, meekness, humbleness)
-jinyenyekeze kwa Mungu, jinyenyekeze kwa kumtii, kumpenda, kumheshimu.
2. Moyo wa kiasi ( sobriety)
-kuwa na kiasi katika kila jambo.
Kila mtu hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe, huku akivutwa na kudanganywa. Tukiwa watii na wenye kiasi hatutadanganywa kiasi cha kuifanya tamaa ichukue mimba na kuzaa dhambi itakayozaa mauti.
OH! HALELUYA!!
UNYENYEKEVU UTAFANYA TUINULIWE JUU, TUKIINULIWA JUU, TUNAKUWA JUU YA FALME NA MAMLAKA, HIVYO TUTAWEZA KUNG'OA, KUBOMOA NA KUHARIBU NA KUANGAMIZA KILA JARIBU NA PITO MBELE YETU, HUKU TUKIJENGA NA KUPANDA UFALME WAKE ALIYE MKUU.

Thursday, 7 April 2016

NGUVU YA MAARIFA


Yohana 1:1-3 "Hapo mwanzo kulikuwako na Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilianyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichoanyika."

Maarifa ni uhalisia, taarifa na ujuzi anaoupata mtu kupitia uzoefu au elimu; ni dhahania au kwa kulitenda jambo.
Maarifa Ni moja kati ya Roho Saba za Mungu.
Maarifa ni muhimu sana kwa mwanadamu, kwani pasipo maarifa uangamivu hutokea,

Hosea 4:6 "Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako."

Hivyo basi, haijalishi ni jambo gani unahitaji kulifanya, kama huna maarifa ya jambo hilo lazima uangamivu au kutofanikiwa kutokee,Katika Yohana 1:3 tunaona kuwa pasipo Neno hakikuanyika chochote, kama Mungu mwenyewe hakufanya chochote pasipo Neno, mimi na wewe je?
Kuwa na maarifa katika jambo husika ni muhimu sana. Hivyo Neno alikuja ili tuwe na maarifa, kisha tupate kuwa na uzima, yaani tuepukane na uangamivu kwa kukosa maarifa.

Yohana 1:14 "Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli."

Yohana 10:10 "Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele."
 
Mtume Paulo pia alihubiri katika Athene;

Matendo 17:23 "Kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua."

aliwapa Neno, ambalo ni maarifa ya kumjua Mungu ambaye watu wa Athene hawakumfahamu.
Swali; Je, kuna mahusiano gani kati ya imani na maarifa?

~tukutane wakati mwingine katika ukurasa huu...~