Tuesday, 21 April 2015

NAMNA YA KUTAMBUA KUSUDI LA KUUMBWA KWAKO






Watu wengi hujiuliza sana, ni namna gani wataweza kutambua kusudi la kuumbwa kwao? Imefikia kipindi wengine wakadhani kuwa vile wanavyoishi ndio kusudi la kuumbwa kwao, hebu fuatana name ili uweze kujifunza namna utakavyoweza kutambua kusudi la kuumbwa kwako;

Kwanza kabisa, kusudi la Mungu kumuumba mwanadamu ni ili kuwa na ushirika (campany), ndio maana katika uumbaji wa Mungu, ni mwanadamu tu ndiye aliyemuumba kwa mfano na sura yake, si wanyama, si mimea, si wadudu wala si malaika.


Mwanzo 1:26 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu;…"


 Hivyo, alimuumba mwanadamu kwa mfano na sura yake ili kupata ushirika. Ndio maana Mungu alikuwa na utaratibu wa kumtembelea mwanadamu aliyemuumba kwa mfano na kwa sura Yake.


Mwanzo 3:8 “Kisha wakasikia sauti ya BWANA Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, BWANA Mungu asiwaone.”


Hii inaonyesha kuwa Mungu alikuwa na utaratibu wa kumtembelea Adamu na mkewe katika bustani aliyowapa ili wailime na kuitunza. Wakati wa jua kupunga ni wakati wa mapumziko, hivyo BWANA Mungu alimtembelea mwanadamu aliyemuumba kwa mfano na sura yake wakati huo kwani alijua kwa wakati huo mwanadamu atakuwa katika mapumziko.


Sasa basi, kama kusudi la kwanza la uumbaji wa Mungu ni kuwa na ushirika na wewe, Je! Utawezaje kuwa na ushirika na Mungu?

Tumeona Mwanzo 3:8 hapo juu inavyoeleza, ni ukweli usiopingika kuwa dhambi huondoa ushirika wa mwanadamu na Mun gu, na ushirika huo ulivunjwa na mwanadamu mwenyewe aliyemuumba kwa mfano na sura yake, tunasoma; “… Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, BWANA Mungu asiwaone” hivyo aliyetoroka na kujificha ili kuharibu ule ushirika ni mwanadamu.

Sasa tunawezaje kurudisha ule ushirika?


Njia ya kurudisha ule ushirika ni moja tu, hakuna njia nyingine zaidi ya hiyo, ni kumpokea Yeye ( BWANA wetu Yesu Kristo wa Nazareth) aliyekubali kujitoa, kuvaa namna ya ubinadamu, kubeba dhambi ya uovu wetu ili sisi tuhesabiwe haki na kurudishiwa ushirika wetu ambao tuliupoteza.


1Timotheo 2:5 “Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Yesu Kristo.”


Labda ni kwa nini anaitwa mwanadamu? Mwana ni mtoto, Adamu ni mtu aliyeumbwa na Mungu, hivyo MWANADAMU ni ufupisho tu wa Mwana wa Adamu, na aliitwa hivyo kwa sababu alikuja ulimwenguni kwa njia ya kuzaliwa na mwanamke.


Na hakuna mwanadamu ambaye hahitaji kumpokea BWANA Yesu, kwani hakuna mwanadamu ambaye hana dhambi;


Warumi 3:23-24 “Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi  ulio katika Kristo Yesu.”


Na dhambi kubwa kuliko zote ni kutompokea Yesu, kutomwanini Yeye, kwani mengine yote tunahesabiwa haki katika Yeye.

Unawezaje kumpokea BWANA Yesu?


Warumi 10:9 “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.”


Na mpango wa wokovu uliandaliwa tangu mwanzo, wakati wa uumbaji, kwani ni utaratibu wa Mungu wetu kutangaza mwisho tangu mwanzo, yaani analiandaa jambo na kuona yale yatakayotokea hadi mwisho wake, kasha anaanza kulitekeleza. Hivyo kabla hajaumba chochote, alishaona hata yale yatakayotendwa na mwanadamu atakaye muumba na mpango wa wokovu ulishaandaliwa, ndio maana Kumbukumbu la torati linafafanua zaidi kuhusu wokovu;


Kumb 26:16-19 “Leo hivi akuamuru Bwana, Mungu wako, kuzifanya amri hizi na hukumu; basi uzishike na kuzifanya kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote. Umemwungama BWANA leo, kuwa ndiye Mungu wako, na kuwa yakupasa kutembea katika njia zake, na kushika amri zake, na maagizo yake, na hukumu zake, na kusikiza sauti yake; naye BWANA amekuungama hivi leo kuwa taifa iliyotengwa iwe yake Yeye, kama alivyokuahidi, na kuwa yakupasa kushika maagizo yake yote; na kuwa atakutukuza juu ya mataifa yote aliyoyafanya, kwa sifa, na jina, na heshima, nawe upate kuwa taifa takatifu kwa BWANA, Mungu wako kama alivyosema”


Hivyo basi, kama hujampokea BWANA Yesu, tafadhali mpokee leo, huwezi kutimiza kusudi la mungu kukuumba iwapo hujampokea Yesu, kwani kumpokea Yesu ni kusudi la kwanza na muhimu kuliko mengine yote.


Kama bado hujampokea Yesu, tafadhali Kiri sala hii;

“Ee BWANA Yesu, ninakuja mbele zako, mimi mwenye dhambi, nipokee leo, nifanye kuwa wako! Lifute jina langu katika kitabu cha hukumu, niandike jina langu katika kitabu cha uzima, Nipe roho wako mtakatifu aniongoze, kutembea na wewe sawasawa, Amina.”


Kwa ukiri wa sala hii amini umeokoka, onana na kanisa lililo karibu nawe linaloamini katika wokovu kwa msaada zaidi wa kiroho au waweza wasiliana nami kwa simu namba 0713469596.

Je, hatua nyingine za kutambua kusudi la kuumbwa kwako ni zipi? Tuonane wakati mwingine.


~BARIKIWA SANA~



No comments:

Post a Comment