Friday, 24 April 2015

KUTAMBUA KUSUDI LA KUUMBWA KWAKO; ~inaendelea~…



Tumeona hatua ya kwanza kabisa katika kutambua kusudi la kuumbwa kwako ambayo ni Kuokoka; karibu tuendelee kufuatilia hatua nyingine za kutambua kusudi la kuumbwa kwako;


Jambo la Pili; Historia ya kuzaliwa kwako;

Historia ya kuzaliwa kwako ni ya muhimu sana, kwani kwa kiasi kikubwa huelezea mwelekeo wako. Ninaposema Historia ya kuzaliwa kwako, haijalishi kuwa historia yako ni mbaya au nzuri, bali pia hubeba kusudi la kuzaliwa kwako. Ni vizuri ukatambua historia yako, kwani ina mchamngo mkubwa sana na itakufumbua macho ni nini cha kufanya au kusudi unalopaswa kulitimiza.

Tunasoma historia ya Yakobo;

Mwanzo 25: 24-26 “Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake. Wa kwanza akatoka, naye alikuwa mwekundu mwili wote kama vazi la nywele. Wakamwita jina lake Esau. Baadaye ndugu yake akatoka na mkono wake unamshika  Esau kisigino. Akaitwa jina lake Yakobo. Isaka alikuwa mwenye miaka sitini mkewe alipowazaa.”


Hosea 12:3 “Tumboni alimshika ndugu yake kisigino; Na alipokuwa mtu mzima alikuwa na uwezo kwa Mungu”


Hii inaonyesha ni namna gani kuzaliwa kwa Yakobo kulileta maana ya kuumbwa kwake, ndiye uzao wa taifa takatifu la Israeli, na alipewa jina hilo kutokana na uwezo aliokuwa nao.


Mwanzo 32:28 “Akamwambia, Jina lako hutaitwa tena Yakobo, ila Israeli, maana umeshindana na Mungu, na watu, nawe umeshinda.”


Tuone pia historia ya Bwana Yesu;

Luka 2:6-7 “Ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia, akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng’ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.”


Tunaona kuwa Bwana Yesu mwenyewe hakupata nyumba wakati anazaliwa, kwa namna ya kibinadamu unaweza kuona kuwa alizaliwa katika mazingira magumu, lakini hii ina maana kubwa sana sawasawa na kusudi lake la kuja ulimwenguni. Ndio maana nimeandika jambo la kwanza kabisa ni kuokoka, kwani ukisharudisha mahusiano yako na Mungu, atakujulisha na kukufunulia yote kwa Roho wake Mtakatifu kwa habari ya historia ya kuzaliwa kwako. Haijalishi iwapo historia yako ni nzuri sana au ni mbaya sana, haijalishi kuwa umezaliwa katika mazingira gani, tambua kuwa historia ya kuzaliwa kwako ina kusudi la Ki-Mungu ndani yake.


Je, unaifahamu vizuri historia ya kuzaliwa kwako? Unalitambua kusudi lililobebwa katika historia hiyo?


Maombi:

“Bwana Yesu, ninakushukuru kwa kuwa Umeniumba kwa kusudi, asante kwa kunipa kufahamu kuwa namna ya kuzaliwa kwangu imebeba pia kusudi la kuumbwa kwangu; Ninakuomba Ee Bwana Yesu, kwa Roho wako Mtakatifu unifunulie yale nisiyoyajua, nipe kulitambua kusudi lililopo kwa namna ya kuzaliwa kwangu, ili nipate kutimiza mapenzi yako, nitie nguvu Bwana na nipe kuufikia mwisho mzuri; Amina.”


Kwa maswali, maoni au ushauri, tafadhali tuwasiliane;
0713469596 au agreyndiwu@gmail.com


Tukutane wakati ujao kwa kuitazama hatua nyingine itakayokuwezesha kutambua kusudi la kuumbwa kwako.


~BARIKIWA SANA~

No comments:

Post a Comment