Bwana Yesu, asante kwa ajili ya siku hii ya leo, ndiwe
uliyenifikisha kwa neema yako, ulinzi wako na uweza wako, Asante Bwana Yesu.
KUOKOKA;
Ni miaka saba sasa tangu nikupokee wewe Bwana Yesu Kristo wa
Nazareth kuwa ni Bwana na mwokozi wa maisha yangu, ni jambo la kukushukuru sana
Mungu wangu uliyenifikisha leo hii.
Ilikuwa ni mwaka 2008, April ya tarehe 27 katika kanisa la
Efatha kituo cha Mwendakasi kilichopo Mwendapole Kibaha, baada ya kupata
mwaliko wa kushiriki ibada ya Jumapili katika kanisa hilo, kutoka kwa kijana
mmoja aitwaye Wille, ambaye alikuwa mshirika wa kanisa hilo pia, na aliwahi
kumsaidia mdogo wangu Godfrey Malifimbo kwa maombi baada ya kusumbuliwa na
tumbo; kama ilivyo utaratibu wake wa ibada, siku hiyo ilikuwa ni ya tofauti
sana kwangu, kwani nilihisi uwepo wa nguvu ya Mungu katika ibada hiyo. Baada ya
ibada kumalizika, ambapo ibada ya siku hiyo iliongozwa na Mchungaji kiongozi wa
kanda(mkoa) wa Kimara, akakaribisha utambulisho wa wageni ambapo mimi, na
wadogo zangu, Godfrey Malifimbo, Justine Luambano na rafiki yetu Hamis Funuki
tulijitambulisha. Baada ya utambulisho ndipo Mchungaji huyo aliita wale ambao
wanataka kumpa Yesu maisha yao, wapiti mbele. Nikiwa nimetulia kwenye kiti sina
wazo la kupita mbele, niliyasikia maneno haya ambayo hayakutamkwa na mtu
yeyote, bali Bwana Yesu mwenyewe alisema nami, “Ukinikataa mbele ya watu, name
nitakukataa mbele za Baba yangu wa Mbinguni” kwa kweli, baada ya kusikizishwa
maneno hayo; niliinuka na kusonga mbele, Oh! haleluya… ndipo Mchungaji huyo
akaniongoza sala ya toba. Kwa wakati huo, nilikuwa sijawahi kusikia Huduma ya
Efatha ni mara yangu ya kwanza, na kuhusu Mtume na Nabii ndio kabisaa, sikuwahi
kumsikia.
BAADA YA KUOKOKA;
Kwa ujumla kwa kipindi hiki chote cha miaka saba, sijawa
mkamilifu mbele zake, sijatembea kwa utakatifu kama ambavyo ilinipasa, lakini
Mungu ni mwema! Nalipokuwa katika hali ya kuzungukwa na uovu, alikuwa mwaminifu
kwangu kujitokeza na kunionya, kunitakasa , kunitia nguvu na kuniridhia kwa
upya, na kuniwezesha kuinuka tena na kusonga mbele.
Baada ya Jumapili hiyo, nikarudi kanisani kwangu nilikokuwa
nikisali (R.C) na sikupenda tena hata kuwasiliana na kaka Yule
aliyetukaribisha, mara nyingi alijitahidi kuja kututembelea shule (Kibaha
Sekondari), bila mafanikio.
Mnamo mwezi Juni, tulikuwa na mapumziko ambapo nilibaki Dar
es Salaam! Nilimshirikisha Mjomba wangu Gaston, kwa habari ya mwaliko
tulioupata kwa Yule kijana name kukubali kumpokea Yesu, ndipo Mjomba akaniambia
Makao Makuu yake yapo Mwenge, na akaniambia tukasali Jumapili, nami nikakubali.
Hatimaye jumapili ikawadia, tukawasili kanisani hapo na
Ibada iliongozwa na Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira, kwa mara ya kwanza
kwangu kuonana na mtumishi huyo wa Mungu. Siku hiyo ilikuwa ni ya ajabu sana
kwangu, kwani kuna mambo mengi ambayo Mungu alisema name nilipokuwa mdogo,
nikayaona mambo hayo yakijidhihirisha siku hiyo kwa macho yangu, mambo hayo
yalihusisha namna ya kutumika, kiasi kwamba sikuwahi kuona yakitendeka kwa
Mtumishi yeyote niliyewahi kumsikia au hata niliokuja kuwasikia baadaye, na
kuanzia wakati huo, MOYO wangu ukaambatana na MOYO wa Mtumishi huyu, nami baada
ya hapo nikafanya shauri kuwa mimi ni wa Efatha name nitatumika pamoja na Mtume
na Nabii Josephat Elias Mwingira. Niliporudi shule, nikaenda kuripoti Kanisani
Mwendakasi na kuanza madarasa ya kukulia wokovu mara moja. Nilimwomba sana
Mungu nifikie ubatizo kabla sijaenda likizo ya Desemba, Mungu ni mwema, mnamo mwezi
Oktoba, nikapata ubatizo. Na mwezi Juni 2009, nikapata ubatizo wa Roho
Mtakatifu baada ya kumaliza masomo ya Kukulia wokovu, (wokovu, ubatizo na Roho
Mtakatifu), asante sana mwalimu wangu wa madarasa ya kukulia wokovu, Mwl. Eliza
kutoka Huduma ya Efatha, kituo cha Mwendakasi, Mungu akubariki sana.
CHANGAMOTO;
Changamoto katika maisha ya wokovu hazikosekani, changamoto
ya kwanza ni mwili, mwili ni dhaifu, na mwili hushindana na roho wakati wote,
ashukuriwe Mungu aliyenipa kuwepo hapa nilipo leo hii.
Changamoto ya pili niliyokutana nayo ni kubaguliwa na baadhi
ya wapendwa kwa sababu tu ya sehemu ninayoabudu, yaani Huduma ya Efatha, lakini
kwa kuwa Yeye ninayemwamini ndiye aliyeniridhia kuwepo mahali hapa, hata siku
moja sijawahi kukata tama kwa ajili ya hili.
Changamoto nyingine ni vikwazo mbalimbali ninavyokutana
navyo katika kutimiza kusudi la Mungu, ikiwa ni pamoja na kukatishwa tama, kutotitimiza
malengo, au wakati mwingine malengo ambayo nimetumaini kuwa ni sahihi kuja
onekana kuwa hayakuwa sahihi.
MAISHA YANGU KWA UJUMLA;
Ninakupenda Bwana Yesu, kwani umekuwa mwaminifu sana kwangu
na hata wakati huu umenizingira kwa utukufu wako mkuu. Umenipa familia kubwa
ambayo imenizingira kwa upendo mwingi;
Umenipa marafiki mbalimbali ambao wamekuwa faraja kubwa sana
kwangu;
Wazazi wangu, Mungu awabariki sana! Kwani mmeniwezesha
kufika mahali hapa.
Kaka zangu na dada zangu, bibi, mamkubwa mamdogo, na
wajomba, nabarikiwa sana nanyi; mchango wenu pia umenifikisha hapa leo hii.
Sauda, wakati wote hakuacha kunijali, hata kama nilikuwa
bize sana na mambo yangu, na sikumjali kwa lolote, hakuchoka wala kukata tama,
bali amezidi kunitazama kwa upendo wako Mungu uliouweka ndani yake, asante.
Tetwigis, wewe ni mtu muhimu sana kwangu, ni kweli
nilikukatika tama hata yametokea yaliyotokea, lakini Mungu ni mwema nabarikiwa
sana na wewe, umekuwa faraja kubwa sana kwangu.
Anko Gaston, you mean a lot to me, Mungu akubariki sana.
Nuru, Sadick, Charlz na Said hakika mmekuwa faraja kwangu,
hata wakati mwingine washauri wazuri kwangu katika wakati niliofikia wa kukata
tama. Keneth, wewe si rafiki tu kwangu, wewe ni ndugu yangu sasa.
Asante pia kwa watu mbalimbali ambao Mungu umewainua na
wamefanyika Baraka kubwa sana kwangu hata kuifikia leo hii, Mwl. Kayombo, Mwl.
Kinunda, Mwl. Ngonyani, Mwl. Kapinga, Mwl. Ndunguru, Mr. A. Salim, Mr.
Kaselenge, Mr. Sweke, Miss Beatrice, Mr. & Mrs. Kattanga, Mrs. Gangisa,
Mrs. Kunyanja, Mr. Mandele na wengine ambao sijaweza kuwaandika hapa, kwa kweli
wamefanyika msaada mkubwa sana kwangu hata leo hii nimefika hapa nilipo. Mungu,
nakusihi zidi kuwainua na kuwabariki sawasawa na walivyomtendea fadhili
Mtumishi wako.
Katika maisha yangu, my Mentors ni Mtume na Nabii Josephat
Elias Mwimgira na Mr. & Mrs Kattanga. Mungu awajalie kutenda vyema na
kuwainua katika viwango vya juu zaidi ili niwe na mengi zaidi ya kujifunza toka
kwenu.
Asante sana Mchungaji Philipo, Mchungaji kiongozi wa Mkoa wa
Ruvuma na Mch. Boniface, wa kituo cha Mbinga, nabarikiwa sana na nyinyi
watumishi wa Mungu.
Kwa hakika Mungu amenishindia na mengi hata leo hii nimefika
mahali hapa, sitaisahau tar 30 Julai, 2012, Mungu aliponiepusha na kifo cha
ajali ya gari kwa namna ya ajabu sana! Amenipigania katika elimu yangu hata leo
hii nimefika mahali hapa. Hakika BWANA wewe ni Yebeneza.
KIUTUMISHI;
Kwa miaka hii saba, namshukuru Mungu amenitumia kwa namna ya
ajabu sawasawa na mapenzi yake, nimesababisha wengine kumpokea Yesu, na wengi
kupata maarifa ya kumjua Yeye, wengine wameponywa na wengine wamefumguliwa!
Asante Bwana Yesu.
USHAURI WANGU;
Hatuendi kwenye makanisa kama fasheni au ufahari, bali ni
kwa sababu Bwana ametukusudia tuwepo mahala tulipo. Hivyo ni lazima ujue mahala
ulipokusudia kuwepo na mlezi wako wa Kiroho. Hii itakusaidia kuwa na msimamo wa
Kiroho na kukuepusha na uzururaji.
Pili; wokovu ni wa mtu binafsi, usiendeshwe na misimamo ya
makundi ambayo inasimama kinyume na imani yako, hata kama kundi hilo ni la watu
aliookoka, mtii Mlezi wako wa Kiroho ambaye Bwana Mungu amekupa.
Tatu; Katika maamuzi yako yote, tanguliza wokovu wako mbele,
yaani usiamue jambo lolote ambalo ni kinyume na wokovu, kinyume na maagizo,
maelekezo na amri za Mungu.
HITIMISHO;
Mungu akubariki sana wewe ambaye kwa namna moja au nyingine
umefanyika Baraka kwangu.
“Ee Bwana Mungu, asante kwa ajili ya neema yako katika
maisha yangu, nakupenda Bwana Yesu, nenda nami Bwana, nipiganie na nishindie
katika safari hii, nikupendeze wewe na niyatende mapenzi yako… Amina!”
Mungu wangu akubariki sana!
MTUMISHI AGREY E. HYERA