Tuesday, 24 November 2015

NURU YA KUKUPELEKA KATIKA KUSUDI LA KUUMBWA KWAKO



Tumetazama hatua nyingi za kullitaambua kusudi la kuumbwa kwako na baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatia, katika toleo lililopita tulijifunza kuhusu kuanza kufanya jambo la kwanza, na tukatazama katika uumbaji wa Mungu kuiwa alianza na NURU katika uumbaji wa ulimwengu na vyote vilivyomo.
Na tuliona kuwa Nuru(Mwanga) ni nini.

Je, nuru hizo ni zipi?
Kama tulivyojifunza katika toleo lililopita kuwa nuru huwezesha kuona, hivyo hata ukiwa na maono, unahitaji nuru ili maono yako yaweze kudhihirika.
Nuru hizo ni mjumuisho wa mambo mengi ambayo wakati wote hukupa hamasa kuwa uliwazalo linawezekana na ni wewe unatakiwa kulituimiza. Hata ukiwa katika kukata tamaa, mambo hayo husimama na kukutia nguvu, na kukufanya uinuke ukiwa na ujasiri tele kisha kuanza tena hata kama uliona umeshindwa.
Mambo hayo ni yepi?

Jambo la kwanza ni nguvu ya Mungu,

Wafilipi 4:13 “Nayaweza mambo yote katika Yeye anitiaye nguvu.”

Katika uumbaji wake, Mwenyezi Mungu alishaweka kila kitu ndani yako kwa ajili ya kukuwezesha kutimiza kusudi lake aliloliweka ndani yako, hivyo kulitimiza kusudi hilo huhitaji mazingira ya nje yakuamulie, kwani uweza wote wa kulitimiza kusudi hilo umo ndani yako,

Waefeso 3:20 “Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu.”

Kila kitu tayari unacho, rasilimali unazohitaji kutimiza malengo yako ambayo ndiyo kusudi la kuumbwa kwako, huvutwa na nguvu ya Kiungu iliyo ndani yako. Mfano: soma historia ya maisha ya Ibrahimu Mwanzo 13:8-9; Ibrahimu alitambua kuwa utajiri wake haumo katika ardhi nzuri, bali ni nguvu iliyo ndani yake ndiyo inayompa utajiri. Vilevile katika historia ya Yakobo, alitoka kwa babaye mikono mitupu lakini alirudi akiwa na utajiri mkuu ambao hakuupata kwa kutarajia mazingira ya nje, bali nguvu ya kuingu iliyo ndani yake ndiyo iliyomfanikishia.

Jambo la Pili, kuwa na mipango.
Hili pia ni jambo muhimu sana katika hatua za kutekeleza kusudi la kuumbwa kwako, ni lazima uwe na mikakati, ujue unatoka wapi, upo wapi na unaelekea wapi. Hii itakupa kutambua ni wapi umekosea na ni nini ukirekebishe, kuna wapendwa wengi wamekuwa wakikurupuka katika utendaji wa mambo wakidhani kuwa wanaweza fanya chochote wakati wowote kwa kuwa wana nguvu ya Mungu. Na imefikia wakati wanmaona kama kupanga si jambo la kiroho, hii si kweli. Mungu ni Mungu wa utaratibu, hata katika uumbaji, tuliona alifanya kila kitu kwa hatua, si kwamba hakuweza kufanya mambo yote kwa siku moja, bali alikuwa akitufundisha kufanya mambo kwa utaratibu.

Luka 14:28 “Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?”

Hii inaashiria kuwa ni lazima tuwe na dira, yaani mipango inayoonesha tunatoka wapi na tunaelekea wapi;

Isaya 46:10 “nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, shauri langu litasimama, name nitatenda mapenzi yangu yote.”

Hii inatudhihirishia kuwa ni utaratibu wa Mungu pia kupanga jambo analolitenda hadi mwisho wake kabla ya kuanza kulitekeleza, Je mimi na wewe?
Anza leo, kuwa na mpango kazi katika kutimiza malengo yako.



No comments:

Post a Comment