Tuesday, 19 May 2015

KUTAMBUA KUSUDI LA KUUMBWA KWAKO; INAENDELEA…






Tumeona hatua mbili  ambazo zitakusaidia kutambua kusudi la kuumbwa kwako, ambazo ni kwanza kuokoka na pili historia ya maisha yako.
Wacha tuendelee kuona hatua nyingine ambayo itakuwezesha kutambua kusudi la kuumbwa kwako;

Historia ya maisha yako/ maisha uliyopitia;

Hii ni hatua muhimu sana katika maisha ya mwanadamu, kwani maisha uliyopitia ni sehemu ya kuandaliwa ili ulitimize lile kusudi la Mungu katika maisha yako. Hakuna jambo a,mbalo limetokea kwa bahati mbaya katika maisha yako, kila jambo limetokea kwa kusudi maalumu, ikiwa ni sehemu ya kuandaliwa kwako;

Hebu tumtazame mfalme Daudi;                                                     

1Samweli 16:21 “Basi Daudi akamwendea Sauli, akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye akapata kuwa mtu wa kumchukulia silaha zake”

1Samweli 17:34-36 “Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija samba, au dubu, akamkamata mwana kondoo wa lile kundi, mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua. Mtumishi wako alimwua samba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai.”

Daudi alikuwa Mfalme maarufu sana na hodari wa vita, ambaye alimpendeza Mungu, hata Bwana Yesu akaitwa Mwana wa Daudi. Kuwa hodari wa vita haikuja tu kwa bahati, alipitia maisha mbalimbali ambayo yalimuandaa kwa ajili ya jukumu hilo. Alianza kupambana na wanyama hatari waliokuwa wakivizia mifugo yake, akaja kuwa mbeba silaha wa mfalme Sauli, hii yote ikiwa ni sehemu ya kuandaliwa.
Hebu tumtazame pia;

Mwanzo 39:4 & 22 “Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake.” “Mkuu wa gerezaa kawatia mkononi mwa Yusufu watu wote waliofungwa, waliomo gerezani; na yote yaliyofanyika humo ndiye aliyeyafanya.”

Utawala wa Yusufu haukuja kwa bahati tu, aliandaliwa, ni utaratibu wa Mungu kukuandaa kabla hajakupa majukumu. Hata Musa nawe aliandaliwa kama mtawala, kwani alichukuliwa katika familia ya kitawala (Farao) ili awe mtawala kwa wana wa Israeli. Je, ni maisha ya namna gani umepitia? Je, umejifunza nini katika maisha hayo? Hata kama maisha uliyopitia ni magumu kama ambavyo Yusufu alipitia, tambua kuwa kuna kusudi la Mungu hapo, kuna jambo unapaswa kujifunza, usipoteze wakati kwa kulaumu watu au kumlaumu Mungu, Mungu ni Mungu wa utaratibu, hutenda kila jambo kwa kusudi maalumu, mwombe Roho Mtakatifu akusaidie kutambua kusudi la Mungu hapo ulipo.

MAOMBI;
“Bwana Yesu, ninashukuru kwa kuniwezesha kuatmbua kuwa maisha niliyopitia na ninayopitia yana kusudi lako ndani yake, nime Roho wako wa Ufahamu anipe kulitambua kusudi lako na Roho wako wa Uweza anisaidie katika kulitimiza kusudi lako. Amina.”
Usikose sehemu inayofuatia katika mwendelezo wa somo hili...

~BARIKIWA SANA~ 

TOLEO MAALUMU; MIAKA SABA YA WOKOVU




Bwana Yesu, asante kwa ajili ya siku hii ya leo, ndiwe uliyenifikisha kwa neema yako, ulinzi wako na uweza wako, Asante Bwana Yesu.

KUOKOKA;
Ni miaka saba sasa tangu nikupokee wewe Bwana Yesu Kristo wa Nazareth kuwa ni Bwana na mwokozi wa maisha yangu, ni jambo la kukushukuru sana Mungu wangu uliyenifikisha leo hii.
Ilikuwa ni mwaka 2008, April ya tarehe 27 katika kanisa la Efatha kituo cha Mwendakasi kilichopo Mwendapole Kibaha, baada ya kupata mwaliko wa kushiriki ibada ya Jumapili katika kanisa hilo, kutoka kwa kijana mmoja aitwaye Wille, ambaye alikuwa mshirika wa kanisa hilo pia, na aliwahi kumsaidia mdogo wangu Godfrey Malifimbo kwa maombi baada ya kusumbuliwa na tumbo; kama ilivyo utaratibu wake wa ibada, siku hiyo ilikuwa ni ya tofauti sana kwangu, kwani nilihisi uwepo wa nguvu ya Mungu katika ibada hiyo. Baada ya ibada kumalizika, ambapo ibada ya siku hiyo iliongozwa na Mchungaji kiongozi wa kanda(mkoa) wa Kimara, akakaribisha utambulisho wa wageni ambapo mimi, na wadogo zangu, Godfrey Malifimbo, Justine Luambano na rafiki yetu Hamis Funuki tulijitambulisha. Baada ya utambulisho ndipo Mchungaji huyo aliita wale ambao wanataka kumpa Yesu maisha yao, wapiti mbele. Nikiwa nimetulia kwenye kiti sina wazo la kupita mbele, niliyasikia maneno haya ambayo hayakutamkwa na mtu yeyote, bali Bwana Yesu mwenyewe alisema nami, “Ukinikataa mbele ya watu, name nitakukataa mbele za Baba yangu wa Mbinguni” kwa kweli, baada ya kusikizishwa maneno hayo; niliinuka na kusonga mbele, Oh! haleluya… ndipo Mchungaji huyo akaniongoza sala ya toba. Kwa wakati huo, nilikuwa sijawahi kusikia Huduma ya Efatha ni mara yangu ya kwanza, na kuhusu Mtume na Nabii ndio kabisaa, sikuwahi kumsikia.

BAADA YA KUOKOKA;
Kwa ujumla kwa kipindi hiki chote cha miaka saba, sijawa mkamilifu mbele zake, sijatembea kwa utakatifu kama ambavyo ilinipasa, lakini Mungu ni mwema! Nalipokuwa katika hali ya kuzungukwa na uovu, alikuwa mwaminifu kwangu kujitokeza na kunionya, kunitakasa , kunitia nguvu na kuniridhia kwa upya, na kuniwezesha kuinuka tena na kusonga mbele.
Baada ya Jumapili hiyo, nikarudi kanisani kwangu nilikokuwa nikisali (R.C) na sikupenda tena hata kuwasiliana na kaka Yule aliyetukaribisha, mara nyingi alijitahidi kuja kututembelea shule (Kibaha Sekondari), bila mafanikio.
Mnamo mwezi Juni, tulikuwa na mapumziko ambapo nilibaki Dar es Salaam! Nilimshirikisha Mjomba wangu Gaston, kwa habari ya mwaliko tulioupata kwa Yule kijana name kukubali kumpokea Yesu, ndipo Mjomba akaniambia Makao Makuu yake yapo Mwenge, na akaniambia tukasali Jumapili, nami nikakubali.
Hatimaye jumapili ikawadia, tukawasili kanisani hapo na Ibada iliongozwa na Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira, kwa mara ya kwanza kwangu kuonana na mtumishi huyo wa Mungu. Siku hiyo ilikuwa ni ya ajabu sana kwangu, kwani kuna mambo mengi ambayo Mungu alisema name nilipokuwa mdogo, nikayaona mambo hayo yakijidhihirisha siku hiyo kwa macho yangu, mambo hayo yalihusisha namna ya kutumika, kiasi kwamba sikuwahi kuona yakitendeka kwa Mtumishi yeyote niliyewahi kumsikia au hata niliokuja kuwasikia baadaye, na kuanzia wakati huo, MOYO wangu ukaambatana na MOYO wa Mtumishi huyu, nami baada ya hapo nikafanya shauri kuwa mimi ni wa Efatha name nitatumika pamoja na Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira. Niliporudi shule, nikaenda kuripoti Kanisani Mwendakasi na kuanza madarasa ya kukulia wokovu mara moja. Nilimwomba sana Mungu nifikie ubatizo kabla sijaenda likizo ya Desemba, Mungu ni mwema, mnamo mwezi Oktoba, nikapata ubatizo. Na mwezi Juni 2009, nikapata ubatizo wa Roho Mtakatifu baada ya kumaliza masomo ya Kukulia wokovu, (wokovu, ubatizo na Roho Mtakatifu), asante sana mwalimu wangu wa madarasa ya kukulia wokovu, Mwl. Eliza kutoka Huduma ya Efatha, kituo cha Mwendakasi, Mungu akubariki sana.

CHANGAMOTO;
Changamoto katika maisha ya wokovu hazikosekani, changamoto ya kwanza ni mwili, mwili ni dhaifu, na mwili hushindana na roho wakati wote, ashukuriwe Mungu aliyenipa kuwepo hapa nilipo leo hii.
Changamoto ya pili niliyokutana nayo ni kubaguliwa na baadhi ya wapendwa kwa sababu tu ya sehemu ninayoabudu, yaani Huduma ya Efatha, lakini kwa kuwa Yeye ninayemwamini ndiye aliyeniridhia kuwepo mahali hapa, hata siku moja sijawahi kukata tama kwa ajili ya hili.
Changamoto nyingine ni vikwazo mbalimbali ninavyokutana navyo katika kutimiza kusudi la Mungu, ikiwa ni pamoja na kukatishwa tama, kutotitimiza malengo, au wakati mwingine malengo ambayo nimetumaini kuwa ni sahihi kuja onekana kuwa hayakuwa sahihi.

MAISHA YANGU KWA UJUMLA;
Ninakupenda Bwana Yesu, kwani umekuwa mwaminifu sana kwangu na hata wakati huu umenizingira kwa utukufu wako mkuu. Umenipa familia kubwa ambayo imenizingira kwa upendo mwingi;
Umenipa marafiki mbalimbali ambao wamekuwa faraja kubwa sana kwangu;
Wazazi wangu, Mungu awabariki sana! Kwani mmeniwezesha kufika mahali hapa.
Kaka zangu na dada zangu, bibi, mamkubwa mamdogo, na wajomba, nabarikiwa sana nanyi; mchango wenu pia umenifikisha hapa leo hii.
Sauda, wakati wote hakuacha kunijali, hata kama nilikuwa bize sana na mambo yangu, na sikumjali kwa lolote, hakuchoka wala kukata tama, bali amezidi kunitazama kwa upendo wako Mungu uliouweka ndani yake, asante.
Tetwigis, wewe ni mtu muhimu sana kwangu, ni kweli nilikukatika tama hata yametokea yaliyotokea, lakini Mungu ni mwema nabarikiwa sana na wewe, umekuwa faraja kubwa sana kwangu.
Anko Gaston, you mean a lot to me, Mungu akubariki sana.
Nuru, Sadick, Charlz na Said hakika mmekuwa faraja kwangu, hata wakati mwingine washauri wazuri kwangu katika wakati niliofikia wa kukata tama. Keneth, wewe si rafiki tu kwangu, wewe ni ndugu yangu sasa.
Asante pia kwa watu mbalimbali ambao Mungu umewainua na wamefanyika Baraka kubwa sana kwangu hata kuifikia leo hii, Mwl. Kayombo, Mwl. Kinunda, Mwl. Ngonyani, Mwl. Kapinga, Mwl. Ndunguru, Mr. A. Salim, Mr. Kaselenge, Mr. Sweke, Miss Beatrice, Mr. & Mrs. Kattanga, Mrs. Gangisa, Mrs. Kunyanja, Mr. Mandele na wengine ambao sijaweza kuwaandika hapa, kwa kweli wamefanyika msaada mkubwa sana kwangu hata leo hii nimefika hapa nilipo. Mungu, nakusihi zidi kuwainua na kuwabariki sawasawa na walivyomtendea fadhili Mtumishi wako.
Katika maisha yangu, my Mentors ni Mtume na Nabii Josephat Elias Mwimgira na Mr. & Mrs Kattanga. Mungu awajalie kutenda vyema na kuwainua katika viwango vya juu zaidi ili niwe na mengi zaidi ya kujifunza toka kwenu.
Asante sana Mchungaji Philipo, Mchungaji kiongozi wa Mkoa wa Ruvuma na Mch. Boniface, wa kituo cha Mbinga, nabarikiwa sana na nyinyi watumishi wa Mungu.
Kwa hakika Mungu amenishindia na mengi hata leo hii nimefika mahali hapa, sitaisahau tar 30 Julai, 2012, Mungu aliponiepusha na kifo cha ajali ya gari kwa namna ya ajabu sana! Amenipigania katika elimu yangu hata leo hii nimefika mahali hapa. Hakika BWANA wewe ni Yebeneza.

KIUTUMISHI;
Kwa miaka hii saba, namshukuru Mungu amenitumia kwa namna ya ajabu sawasawa na mapenzi yake, nimesababisha wengine kumpokea Yesu, na wengi kupata maarifa ya kumjua Yeye, wengine wameponywa na wengine wamefumguliwa! Asante Bwana Yesu.

USHAURI WANGU;
Hatuendi kwenye makanisa kama fasheni au ufahari, bali ni kwa sababu Bwana ametukusudia tuwepo mahala tulipo. Hivyo ni lazima ujue mahala ulipokusudia kuwepo na mlezi wako wa Kiroho. Hii itakusaidia kuwa na msimamo wa Kiroho na kukuepusha na uzururaji.
Pili; wokovu ni wa mtu binafsi, usiendeshwe na misimamo ya makundi ambayo inasimama kinyume na imani yako, hata kama kundi hilo ni la watu aliookoka, mtii Mlezi wako wa Kiroho ambaye Bwana Mungu amekupa.
Tatu; Katika maamuzi yako yote, tanguliza wokovu wako mbele, yaani usiamue jambo lolote ambalo ni kinyume na wokovu, kinyume na maagizo, maelekezo na amri za Mungu.

HITIMISHO;
Mungu akubariki sana wewe ambaye kwa namna moja au nyingine umefanyika Baraka kwangu.
“Ee Bwana Mungu, asante kwa ajili ya neema yako katika maisha yangu, nakupenda Bwana Yesu, nenda nami Bwana, nipiganie na nishindie katika safari hii, nikupendeze wewe na niyatende mapenzi yako… Amina!”
Mungu wangu akubariki sana!
MTUMISHI AGREY E. HYERA