Kutofanikiwa nkatika jambo lolote ni dalili tosha ya kutokuwa na Mungu, yaani kuyatenda mambo pasipo maongozi ya Roho Mtakatifu.
Hesabu 23:19 "Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?"
Ili kufanikiwa kulitumikia kusudi la kuumbwa kwako, inategemea sana na maamuzi yako na namna unavyoenenda. Watu wengi wamejikuta wakitembea duniani hadi mauti ikiwafikia pasipo kujua ni nini hasa walipaswa kutenda.
Katika makala zilizopita tuliona namna mtu anaweza kulitambua kusudi la kuumbwa kwake, leo tunaendelea na namna ya kulitimiza kusudi hilo baada ya kulitambua;
1. KUTENGANISHA KATI YA MAMBO YALIYO YA HAKI NA MAOVU.
Katika toleo lililopita tuliona umuhimu wa maarifa katika kusudi unalopaswa kulitimiza, katika hatua hiyo ya kuwa na maarifa, pia ni muhimu sana kutambua mambo yaliyo ya haki na yasiyo ya haki. Ni vyema kujitenga na uovu tangu mwanzo, kwani mwanzo ndio msingi ambao unaonesha mwelekeo wa kule unaelekea.
Kutojitenga na uovu itakupelekea kutokuwa na mwisho mzuri, kwani huwezi pata jengo zuri la nyumba toka katika msingi mbovu. Hii ni pamoja na marafiki wasiofaa, na kila jamii ambayo itakupelekea kuanko uharibifu. Ndio maana hata katika uumbaji, baada ya Bwana Mungu kuziumba Mbingu na Nchi, hatua iliyofuata ni kutenganisha kati ya nuru na giza, tunasoma;
Mwanzo 1:1-5 "Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji. Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru. Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema; Mungu akatenga nuru na giza. Mungu akaiita nuru Mchana, na giza akaliita Usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku moja."
2. KUTENGANISHA MAMBO MAKUBWA NA MADOGO/MUHIMU NA YA KAWAIDA.
Mwanzo 1:6-8 " Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji. Mungu akalifanya anga, akayatenga yale maji yaliyo juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo. Mungu akaliita lile anga Mbingu. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya pili."
Ni lazima ujue kutofautisha kati ya mambo ya juu (makubwa/muhimu) na yale ya chini (madogo/ya kawaida)
~tuonane katika toleo lijalo~