ROHO
Roho ni mtu
halisi, ndio maana uhai wa mtu ni roho, kwani iwapo roho itatengana na mwili, mwili hauna kazi tena, ndipo huitwa marehemu na mwili huo huzikwa. Na endapo mtu atakatika mkono, au mguu au kiungo kingine chochote na roho yake ikawa bado, basi mtu huyo atakuwa hai. Tunasoma;
Mwanzo 2:7 "Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai."
Kilichofanya mtu aliyeumbwa kuwa hai ni pumzi ya Mungu, ambayo ndiyo huitwa Roho. Roho ina sehemu kubwa sana, kwani ndiyo hutuunganisha na Mungu wetu, hutuwezesha kupokea yale Mungu ametukusudia na kufanya ibada na Mungu wetu.
NAFSI
Hapo juu tumesoma kuwa mtu huyo akawa nafsi hai. Je, nafsi ni nini?
Nafsi ni
sehemu ambayo huhusika na kuhifadhi maarifa, ni sehema ambayo humfanya mtu aweze kufikiri na kuhifadhi kumbukumbu. Sehemu hii ni kama CPU kwenye kompyuta au Injini ya gari. Tunasoma;
Mwanzo 1:28 "Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kutiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi."
Kilichopewa uwezo wa kutawala ni nafsi, na si mwili, kwani kama ni mwili, kuna viumbe wengi ambao wana nguvu kuliko mtu, bali kwa uwezo wa nafsi, ambako ndiko kuna maarifa, mtu huweza kutawala hata viumbe vyenye nguvu za ajabu.
MWILI
Mwili ni
nyumba ya roho na nafsi, nyumba ya Roho Mtakatifu, ni kiunganishi cha mazingira
ya ndani na nje. Mwili ni sehemu ya utekelezaji wa yale Roho imepokea toka kwa Mungu na yakahifadhiwa katika nafsi, kwa kufuata utaratibu unaotakiwa, nafsi huuamrisha mwili kutekeleza.
Sehemu zote tatu hutegemeana hivyo mwonekano wako kwa ujumla ni matokeo ya roho, nafsi na mwili wako ulivyo.