Tumeona baadhi ya mambo yatakayokuwezesha kutambua kusudi
la kuumbwa kwako, mambo hayo yote ni muhimu sana katika kutambua na kutekeleza
kusudi la Mungu juu ya maisha yako, hivyo ni vyema ukatilia maanani kila
kipengele ili uwe bora na utende kusudi la Mungu kwa ubora hata kufikia mwisho
mzuri kama ambavyo Mtume Paulo alifikia. Hebu tuendelee kuangalia njia nyingine
itakayokuwezesha kutambua kusudi la kuumbwa kwako.
Mwito
wa Ndani;
Hii pia ni sehemu muhimu sana, sehemu hii inajumuisha
jambo lile ambalo unaguswa/unapenda kulifanya. Ndani yako unajisikia furaha
iwapo jambo hilo litafanikiwa, ni jambo lile ambalo lipo akilini mwako. Ndipo
mwandishi wa Zaburi akasema;
Zaburi
19:14 “Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele
zako, Ee BWANA, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.”
Hapa inaonyesha kuwa kuna jambo ambalo mwandishi wa
Zaburi alikuwa akiwaza kulifanya, hivyo alikuwa akimsihi Mungu aliridhie jambo
hilo. Pia tunasoma katika Mithali;
Mithali
16:1 “Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa BWANA.”
Hii inaonyesha kuwa kuna jambo ambalo mwanadamu anawaza
kulifanya, cha muhimu kutambua hapa ni kuwa jambo lile unawaza kulifanya, ni
lazima liendane na mpango wa Mungu, kwani ndiye anayetoa kibali na kuwezesha
jambo hilo litimie, ndio maana nimeeleza kuwa hatua zote nilizozielezea ni
muhimu sana katika kutimiza kusudi la kuumbwa kwako. Tunasoma pia katika kitabu
cha Nabii isaya;
Isaya
43:26 “Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako.”
Bado inaonyesha kuwa tuna nafasi ya kutenda kile
tunawaza, cha muhimu ni kuwa lazima kikubalike na Mungu. Tatizo watu wengi
hawamshirikishi Mungu kwa mabo ambayo wanaguswa kuyafanya, wakidhani kuwa jambo
la Mungu ni lile ambalo ataagizwa na Mungu mwenyewe kulifanya. Iwapo umefuata
hatua ya kwanza ya kumpokea Bwana Yesu, ina maana kuwa maisha yako umeyarejesha
katika mpango wa Mungu, hivyo kila unachokifanya, unakifanya kwa kusudi la
Mungu, ndipo Mtume Paulo akasema;
Wafilipi
1:21a “Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo,…”
Baada ya kumpokea Yesu, Mtume Paulo anatudhihirishia kuwa
mfumo mzima wa maisha yake ulibadilika na kila alilokuwa akilitenda, alikuwa
akilitenda kwa ajili ya Bwana Mungu, sawasawa na vile Mungu mwenyewe alitaka.
Yamkini kuna jambo unawaza kulitenda ila unasita sita
kwani huna uhakika iwapo ni mpango wa Mungu au la, napenda kukutia moyo siku
hii ya leo kuwa acha kusitasita, isikize sauti ya Mungu inayosema ndani yako.
Maombi;
“Ee
Bwana Yesu, niwezeshe Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, yawe
sawasawa na mpango wako juu ya maisha yangu. Amina!”
~Barikiwa
sana!~